Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti mashuhuri wa Jaafari nchini Lebanon, alitoa tahadhari kuhusu hatari inayoikabili Mashariki ya Kati katika hotuba yake ya Swala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Imam Hussein (a.s.), ulioko eneo la Burj al-Barajneh.
Sheikh Qabalan alisema kuwa; Mashariki ya Kati kwa sasa inakabiliwa na fitina hatari zaidi ya “Kimarekani-Kizayuni-Kiulaya”. Alisisitiza kwamba ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuchukua msimamo ulio wazi na madhubuti dhidi ya mradi huo wa kuchochea fitina, ambao Washington inauongoza kwa uratibu wa siri na Tel Aviv pamoja na Brussels, kwa lengo la kuyachonganisha mataifa ya Kiislamu na kuyafanya yapigane yenyewe kwa yenyewe, huku wakichochea moto wa vita vya pande zote ambao hautawezekana kwa yeyote kuuzima na ambao hatimaye utasababisha uharibifu wa kudumu.
Saudi Arabia ichukue nafasi ya “ndugu mkubwa” kuzuia fitina na ukandamizaji wa kimataifa na kikanda
Akiuhutubia uongozi wa Saudi Arabia, Mufti Qabalan alisema: “Hijaz, ardhi yaharamu mbili tukufu, ni chimbuko la Utume na mahali pa ibada, thamani hizi za kipekee zinaitaka Saudi Arabia kutekeleza jukumu la ‘baba halisi’ wa mahusiano yanayoongozwa na Qur’ani; yaani, kuchukua nafasi ya ‘ndugu mkubwa’ ili kuzuia fitina yoyote na kukabiliana na aina yoyote ya utawala dhalimu wa kimataifa au kikanda.”
Aliongeza kuwa, hilo ndilo jambo wanaloliomba kutoka Saudi Arabia, na kwa mujibu wa mantiki ya Qur’ani, ni hitaji la msingi kwa ajili ya uhai na usalama wa eneo hilo.
Alisema Iran, Uturuki, Pakistan, Misri, Iraq, Yemen, Syria na Lebanon zinapaswa kuungana ili kuunda muungano mmoja ulio imara dhidi ya utawala wa Kimarekani-Kizayuni katika Mashariki ya Kati. Alieleza kuwa msingi mkuu wa muungano huo unapaswa kuwa “maslahi ya Waarabu na Waislamu”.
Alionya kwamba; iwapo ushirikiano wa Kiislamu kati ya nchi za Kiislamu hautaundwa, matokeo yake hayatakuwa mengine isipokuwa maafa, uhasama, vita na uharibifu, ambao hautaathiri nchi moja tu, bali utaukumba moyo mzima wa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Aidha, alisema Washington inalenga kuitawala Mashariki ya Kati na kuigeuza kuwa mtandao wa kambi za kijeshi, kwa lengo la kupora nishati, uchumi na rasilimali za kifedha za eneo hilo. Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuzuia mataifa ya Kiislamu kufikia umoja na kuchukua nafasi ya uongozi katika mfumo wa kimataifa.
Sheikh Qabalan alibainisha kuwa; wakati wa sasa unafaa sana kuchukua hatua, hususan kwa kuwa Marekani, baada ya vita vyake na Iran, inakabiliwa na hali dhaifu zaidi katika historia yake na imeathiriwa na udhaifu wa kimuundo katika uwezo wake wa kimkakati.
Alisema suluhisho ni kuunda mfumo wa usalama wa kikanda unaojumuisha nchi za Kiarabu na Kiislamu, alionya kuwa uzembe katika kipindi hiki unaweza kusababisha maafa, kwa sababu huu ni wakati wa kutafuta njia za kuendelea kuwepo na kuimarisha nguvu.
Muqawama wa Lebanon ni mfano mkuu zaidi wa kuishinda Israel katika nusu karne iliyopita
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Qabalan alisema: “Ninazungumza na Waarabu kwa ukweli na upendo, nikisema kwamba katika historia ya kisasa ya Waarabu na nchi za Kiislamu, hakuna nguvu iliyoweza kukabiliana na mradi wa Kimarekani-Kizayuni kwa kiwango kinacholingana na nguvu ya wananchi wa Lebanon.”
Alisisitiza kuwa; muqawama wa Lebanon umekuwa mfano mkuu zaidi wa kuishinda Israel katika kipindi cha nusu karne iliyopita, hususan katika vita vya hivi karibuni vilivyotokea baada ya Operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa.
Aliongeza kuwa; tangu mwaka 2006, Washington imekuwa ikijitahidi kuidhoofisha Israel, na kwa sasa inalenga kuiondoa Lebanon pamoja na uwezo wa muqawama wake, ili iweze kutekeleza mipango yake ya kuimeza na kuitawala Mashariki ya Kati.
Sheikh Qabalan alisema kuwa muqawama wa Lebanon unachotaka ni umoja wa Waarabu na Waislamu kwa lengo la kulinda eneo hilo dhidi ya mipango ya Kimarekani-Kizayuni, alisisitiza kuwa; ukweli huu muhimu unapaswa kueleweka wazi na mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu.
Saudi Arabia inapaswa kuwa mshirika na ndugu wa Iran, Iraq, Misri, Lebanon, Yemen na mataifa mengine ya Kiislamu
Mufti Qabalan aliendelea kusisitiza kwamba: Waarabu hawahitaji chochote zaidi ya ushirikiano na uhuru wa kweli, alisema Saudi Arabia inapaswa kuwa mshirika na ndugu wa Iran, Iraq, Misri, Lebanon, Yemen na mataifa mengine ya Kiislamu. Alieleza kuwa lengo lao ni kuzima moto wa fitina inayochochewa na Marekani, Ulaya na Wazayuni katika eneo hilo.
Aidha, alitoa tahadhari kwa kusema: “Yatazameni mataifa haya katika historia yake. Wakoloni wa leo wanafanya mashambulizi kwa ukali zaidi kuliko hapo awali, lengo lao ni mafuta, utajiri na rasilimali za Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, vinginevyo chaguo lao pekee ni kuchochea fitina, kuwasha moto wa vita na kusababisha uharibifu.”
Alisisitiza kwamba; mataifa yenye nguvu katika eneo hilo yanapaswa kuchukua msimamo wa kihistoria kabla hayaja chelewa. Aliongeza kuwa uwepo wa Marekani na Ulaya katika eneo hilo ni kikwazo kikubwa kwa usalama, utajiri na ushirikiano wa Kiislamu.
Sheikh Qabalan alisisitiza kuwa; suluhisho ni kusimamisha moto wa vita, badala ya kuuchochea, alieleza pia kuwa Yemen ni ndugu na mshirika wa Saudi Arabia na Waislamu wengine, alisema kuwa badala ya kuendeleza vita mataifa ya eneo hilo yanapaswa kuelekea katika kujenga upya mfumo wa kikanda.
Mwisho, aliwakumbusha waumini kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’ani Tukufu isemayo:
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ
“Hakika waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kurehemewa.”
Maoni yako